Tuesday, 12 August 2014

HONGERA MWALIMU WANGU







 





















Bila shaka lizitia, za mchwa tena bidii
kujimudu na kukua, uniwezeshe muradi
andika na kuongea, lugha iliyo mufti
Hongera mwalimu wangu, Mola akujaalie

Linitandika viboko, kidhani hukunipenda
kumbe mkubwa upendo, nao kwangu ulikuwa
nishike yote mafunzo, na hata kuyakumbuka
Hongera mwalimu wangu, Mola akujaalie

Zangu kazi sahihisha, hala ukazidurusu
moyo wewe ukanipa, darasani zote siku
hata hukukosa moja, lengo lako nifaulu
Hongera mwalimu wangu, Mola akujaalie

Wavyele kawahimiza, nunua vitabu vyote
na sasa nimeibuka, wa kutajika malenge
langu ni kuomba dua, baraka Mungu akupe
Hongera mwalimu wangu, Mola akujaalie

MWANAMKE KISIRANI

MWANAMKE KISIRANI
Kipi kinachokukere, ewe dada mwanamke
wakati wote kelele, ugomvi mwenyeji wewe
huoni waudhi wote, tabia iyo na wewe
Mwanamke kisirani, badili zako hulka

Kwa wakubwa na wadogo, huna haya asilani
hapa pale vijimambo, kusisitiza huishi
muradi kuzua kero, kote kote kiamboni
Mwanamke kisirani, badili zako hulka

Utu kapeleka wapi, manake umepotoka
kuelewa maadili, wewe yakupasa sana
wakwezo huwatambui, hata kidogo angaa
Mwanamke kisirani, badili zako hulka

Maneno wewe ropokwa, siku na wakati wote
muda wote umenuna, hucheki yule yeyote
meoza na unanuka, hufai wote wengine
Mwanamke kisirani, badili zako hulka

Mie nafika tamati, muda 'menipa kisogo
zangu zote nasahi, tilia manani mno
usije ukashtuki, ulimwenguni si pako
Mwanamke kisirani, badili zako hulka

MAJUTO MJUKUU

MAJUTO NI MJUKUU HUJA BAADA YA KITENDO

Alikwishasema babu, kabla ya kuaga kwake
hakusikilizwa katu, hata na yeyote yule
kazeeka mtu huyu, walisema watu wote
Majuto haya makuu, baada hiki kitendo

Simtaki kwangu hapa, mwanamke huyu kero
juu chini hapa fanya, aondoke kwangu hapo
sababu zake tabiya, ni potovu si kidogo
Majuto haya makuu, baada hiki kitendo

Manani ungetiliwa, ushauri huo wake
haya yasingeshuhudiwa, katika aila yake
migogoro zote saa, kisa huyo mwanamke
Majuto haya makuu, baada hiki kitendo

Funzo hasa tena zuri, wote wasiosikiya
wosia wao mzuri, hao waliozeeka
mimi kweli kasadiki, mengi babu kayaona
Majuto haya makuu, baada hiki kitendo



Sunday, 20 July 2014

WAZAZI BARAKA KWANGU
 

Cha kwanza mie kunena, Jalai namshukuru
Pendo amedhihirisha, kwangu niliye muovu
Wazazi kanijalia, jali maslahi yangu
Wavyele hongera sana, duangu aushi ndefu

Lengo niishi na nyinyi, kwa karibu nitembee
Nihakiki mefurahi, wala msikasirike
Yule takayewaudhi, mara moja angamie
Wavyele hongera sana, duangu aushi ndefu

Nia yangu siku moja, sote pamoja tuwepo
Kusiwepo kutengana, wala litenganishalo
Niwe kuwahudumia, kwa vyovyote mtakavyo
Wavyele hongera sana, duangu aushi ndefu

Nafika kikomo mie, sifa nyie nawapeni
Muendeleeni vile, iwe isiwe ni mimi
                                                     Neema Mola tawape, kwa mtendayo mazuri
                                                     Wavyele hongera sana, duangu aushi ndefu

Thursday, 29 May 2014

Nampenda ila kusema ngoma



Nampenda ila kusema ngoma

Ipo nia ya kunena, bali mie naogopa
Kwake iwe nia mbaya, basi vipi itakuwa
Hata zaidi huenda, moyoni  kasononeka
Yeye mno namuenzi, kwangu kusema ni ngoma

Pindi aniangalipo, nia anayo nahisi
Siwezi  jua iwapo, kawaida yake hali
Mie nimuangalipo, nambeza kwa yakini
Yeye mno namuenzi, kwangu kusema ni ngoma

Kutaka kunena naye, aghalabu hunijia
Mbiombio mimi kwake, nimfikiapo ila
Wangu mwili wateteme, nisijue la kunena
Yeye mno namuenzi, kwangu kusema ni ngoma

Kikomo wino natiya, naamini ipo siku
Mrembo takuja sema, nakupenda mwenzi wangu
Waniambiya mtima, yenyewe ipo karibu
Yeye mno namuenzi, kwangu kusema ni ngoma

Friday, 25 April 2014

DUNIA CHAFU IMEWACHAFUA

 Mtima wasononeka, pindi niwazawazapo
Yale ninayoyaona, kote nijivinjaripo
Imegeuka dunia, yatisha uionapo
Jamaneni mambo gani, yameikumba dunia

Dada zanguni vyuoni, nawaomba nisikiye
Usherati mwashiriki, hamjui hatariye
Hamnazo jitieni, lakini mtajutie
Jamaneni mambo gani, yameikumba dunia

Mavazi yenu maovu, yamekosa maadili
Mwavutia dhana yenu, mngalijua laiti
Ukimwi u juu yenu, kumaliza halaiki
Jamaneni mambo gani, yameikumba dunia

Mie kikomo nafika, wakati kwangu adimu
Sitasita kuwaonya, badilika juu yenu
Lau msiposikiya, kaburini mtadumu
Jamaneni mambo gani, yameikumba dunia