Friday, 25 April 2014

DUNIA CHAFU IMEWACHAFUA

 Mtima wasononeka, pindi niwazawazapo
Yale ninayoyaona, kote nijivinjaripo
Imegeuka dunia, yatisha uionapo
Jamaneni mambo gani, yameikumba dunia

Dada zanguni vyuoni, nawaomba nisikiye
Usherati mwashiriki, hamjui hatariye
Hamnazo jitieni, lakini mtajutie
Jamaneni mambo gani, yameikumba dunia

Mavazi yenu maovu, yamekosa maadili
Mwavutia dhana yenu, mngalijua laiti
Ukimwi u juu yenu, kumaliza halaiki
Jamaneni mambo gani, yameikumba dunia

Mie kikomo nafika, wakati kwangu adimu
Sitasita kuwaonya, badilika juu yenu
Lau msiposikiya, kaburini mtadumu
Jamaneni mambo gani, yameikumba dunia